Wilbroad Slaa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). |
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa amesema Serikali imekuwa dhaifu katika kupambana na biashara ya dawa za kulevya hali inayosababisha vijana kuendelea kujiingiza katika uhalifu huo..
Dk Slaa amesema hayo hivi karibuni alipomkaribisha
nyumbani kwake, Padri John Wootherspon kutoka Hong Kong aliyekuja
kuhimiza kampeni ya kuwazuia vijana kuacha kusafirisha dawa hizo katika
majimbo ya China ya Guangzhou, Macau na Hong Kong.
Padri Wotherspon ambaye anawatembelea wafungwa
katika magereza ya Hong Kong, Macau na Guangzhou alisema kwa sasa kuna
wafungwa wa Kitanzania zaidi ya 130 wanaotumikia vifungo kutokana na
kusafirisha dawa za kulevya.
“Nitahakikisha kuwa unafanyika utaratibu wa
kuwaondoa Watanzania waliofungwa Hong Kong warudishwe na kuhukumiwa
nyumbani. Hilo jambo nitalipa kipaumbele kwa nafasi yangu,” alisema Dk
Slaa.
Kuhusu wajibu wa Serikali katika kupambana na
biashara hiyo, Dk Slaa alisema bado kuna udhaifu mkubwa kwani hakuna
mwamko wa dhati wa kuwahukumu kisheria wanaosafirisha dawa za kulevya.
“Ikiwa Umoja wa Mataifa umekubali na kuidhinisha
kuwa wafungwa wanaokamatwa nje ya nchi wahukumiwe katika nchi zao, iweje
leo hapa nchini tusifanye mchakato wa kuwarudisha nyumbani hao ndugu
zetu?” alihoji Dk Slaa.
Katika mkutano huo, Dk Slaa aliandika ujumbe mfupi
wa maneno kwa wafungwa hao akiwatakia maisha marefu na kuwaombea
kumaliza salama vifungo vyao.
“Wadogo zangu, ndugu, dada na kaka zangu, kupitia
Father John, nawaombea kwa Mungu awape ustahimilivu na atawaokoa kwa
uwezo wake. Tupo nanyi,” ulisema ujumbe wa Dk Slaa.
Dk Slaa pia alisoma barua za wafungwa hao zilizoandikwa kwa mkono.
Padri Wootherspon alisema kukutana na Dk Slaa ni sawa na kukutana na kiongozi kama; Nelson Mandela au Mwalimu Julius Nyerere.
“Kwa dakika 90 nilizokaa pale na Dk Slaa
nilijisikia kama nipo nyumbani kwa Mandela au Nyerere. Ninachoomba ni
kuwa kwa nafasi yake asaidie vijana kuacha kusafirisha dawa za kulevya,”
alisema.
Padri Wootherspon ambaye ameondoka jana kuelekea
Hong Kong alisema ataendelea kufanya kila awezalo ili Tanzania isiwe
kichochoro cha kusafirisha dawa za kulevya.
Credit; Mwananchi
Credit; Mwananchi
0 comments :
Post a Comment