Mwenyekiti wa chama cha NCCR Mageuzi James Mbatia (kushoto) akiteta jambo na Mwenyekiti mwenza wa TLP Augustin Mrema. |
Vita ya ubunge baina ya wenyeviti wawili wa vyama vya upinzani, James Mbatia na Augustine Mrema imezidi kupamba moto baada ya kushambuliana bungeni kuhusu kusigana kwenye harakati za ubunge wa Jimbo la Vunjo..
Kwenye vikao vya Bunge na nje, Mrema, mwenyekiti
wa TLP, amekuwa akimlalamikia Mbatia (NCCR-Mageuzi) kuwa anamuingilia
kwenye jimbo lake, lakini juzi alikwenda mbali zaidi alipoomba
kuwasilisha taarifa ya hali yake kiafya na kutumia nafasi hiyo
kumshambulia mpinzani wake, ambaye pia jana aliomba nafasi kama hiyo
kujibu mapigo.
Msuguano wa wawili hao, ambao waliwahi kuwa pamoja
kwenye Chama cha NCCR, ulitokana na uamuzi wa Mbatia kutangaza nia ya
kugombea ubunge wa Vunjo, jimbo ambalo kwa vipindi viwili limekuwa chini
ya Mrema.
Mrema ambaye pia amewahi kuwa mbunge
wa Jimbo la Temeke, alisoma taarifa hiyo ya hali yake ya afya akisema
kuwa yeye si mgonjwa kama inavyodaiwa na atagombea tena ubunge kwenye
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Katika taarifa yake aliyoimbatanisha na ripoti za
madaktari kuhusu vipimo alivyofanya na ambayo alitumia dakika 15
kuisoma, Mrema alimtuhumu Mbatia kwamba amevamia jimbo hilo na kuwaambia
watu wasiwachague wagombea wa TLP, akiwamo na yeye (Mrema) kwa sababu ni
marehemu mtarajiwa, ana saratani na Virusi vya Ukimwi.
Akieleza jinsi Rais Jakaya Kikwete na Spika Anne
Makinda walivyofanikisha safari zake za kwenda nchini India, kuchunguzwa
afya yake, kutibiwa saratani ya mapafu pamoja na kupima Ukimwi, Mrema
alisema: “Awali nilikuwa na saratani ya mapafu, lakini baada ya kupata
matibabu kwa mwaka mmoja, nimepima tena na ripoti za madaktari
zinaonyesha kuwa nimepona.
“Nilipima na ukimwi na vipimo vimeonyesha sina
maambukizi yoyote. Kweli Mungu mkubwa. Hafi mtu hapa. Mimi ni mzima wa
afya na nitagombea ubunge maana ndiyo unanitoa roho.”
Hata hivyo, Mbatia, ambaye ni mbunge wa kuteuliwa
na Rais, jana jioni alikanusha madai hayo bungeni akisema hayana ukweli
wowote.
Credit; Mwananchi
Credit; Mwananchi
0 comments :
Post a Comment