Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju (katikati) akizungumza na viongozi pamoja na wahariri. |
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju amesema madai ya wadau ya kutaka Tume Huru ya Uchaguzi, mgombea binafsi na haki ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais mahakamani, yatafanyiwa kazi iwapo Katiba Inayopendekezwa itapitishwa kwenye Kura ya Maoni Aprili 30..
Jambo hilo ni mtihani mgumu kwa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) ambao umetangaza kususia kuipigia kura Katiba
Inayopendekezwa huku ikitaka mambo hayo matatu yafanyiwe kazi kabla ya
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Katika mazungumzo yake na wahariri na viongozi wa
magazeti Masaju pia alitumia
takribani saa mbili kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu suala la kuanzishwa
kwa Mahakama ya Kadhi.
Masaju
alisema mambo hayo ni muhimu sana katika kipindi hiki na hivyo ni
muhimu kwa wananchi kupitisha Katiba Inayopendekezwa ili masuala hayo
yaandaliwe utaratibu wa kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.
Katika mkutano wa pamoja na Rais uliofanyika
mwishoni mwa mwaka jana, vyama vya upinzani, vikiongozwa na Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), vilitoa hoja ya kutaka mchakato wa Katiba
Mpya uahirishwe hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba na kwamba katika
kipindi hiki Katiba ya sasa ifanyiwe marekebisho ili Tume ya Uchaguzi
iwe huru, kuingiza mgombea binafsi na haki ya kupinga mahakamani matokeo
ya uchaguzi wa Rais.
“Mambo haya matatu yametambuliwa Katiba
Inayopendekezwa na tunaweza kuyawekea mfumo wa kisheria ili yatekelezwe
kama Katiba Inayopendekezwa itakuwa imepitishwa. Kama itapitishwa Aprili
30 na Uchaguzi Mkuu ni Oktoba, halafu tukiiweka Katiba hii kabatini
(tusiitumie), tutapata shida,” alisema Masaju, ambaye aliisifu Katiba
Inayopendekezwa kuwa ina mambo mengi mazuri.
“Ushauri wangu kwa Serikali, kama Katiba imepigiwa kura na watu wakaipitisha, basi tuanze kutekeleza yale yanayowezekana.”
Akizungumzia kipindi cha mpito cha miaka minne
ambacho kimewekwa kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa Katiba hiyo alisema
si lazima Katiba Inayopendekezwa ianze kutumika baada ya kipindi hicho.
“Huo ni muda tu umewekwa na si lazima ufike. Kuna
mambo ya msingi ya kuzingatia. Mfano, Katiba hii imezungumzia masuala ya
haki mbalimbali. Haki hizi utekelezaji wake utategemea na bajeti
iliyopo. Jambo hili linahitaji muda kidogo. Kuna mambo ambayo hatuwezi
kuyafanya kwa sasa, mfano ni hili la haki ya wananchi kupata maji au
kuwa na zahanati kwa kuwa linahitaji bajeti kuliandaa,” alisema.
Pia yale ambayo yanahitaji bajeti kidogo au
kutohitaji kabisa, kama suala la kuwapo kwa Tume Huru ya Uchaguzi,
yanaweza kuanza kutekelezwa.
“Katiba ikipita kuna mambo tunayoweza kuyafanya
hasa yale yanayohusu uchaguzi. Ni mambo ya msingi sana ambayo kama
mkiyaacha watu watawashangaa,” alisema.
0 comments :
Post a Comment