Ndege ya Kenya ikiwa katika maegesho yake ndani ya uwanja wa Jomo kenyatta nchini Kenya. |
Serikali ya Tanzania imesema
itawasiliana na Serikali ya Kenya ili kulipatia ufumbuzi tatizo la
magari ya wafanyabiashara wa Tanzania ambayo
yamezuiwa kuingia kwenye
Uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta nchini Kenya kupeleka na kuchukua
wageni.Kwa mujibu wa baadhi ya wafanyabiashara wa Tanzania ambao wanafanya biashara hiyo wamesema magari yao yalizuiwa na maafisa wa Kenya tangu Desemba 22 mwaka jana kwa madai kwamba ni amri kutoka ngazi za juu za utawala wa Serikali ya Kenya.
Mmoja ya watanzania anayemiliki magari yanayofanya biashara ya kubeba na kupeleka wageni katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta nchini Kenya Moses King'ori siku ya zuio hilo magari yao yalipofika katika lango la Uwanja wa ndege yaliambiwa hayaruhusiwi kuingia.
Kufuatia zuio hilo la magari ya wafanyabiashara wa Tanzania, serikali ya Tanzania kupitia kwa Waziri wa Maliasili na utalii Lazaro Nyalandu amesema wanawasiliana na serikali ya Kenya ili kulipatia ufumbuzi sakata hilo.
Kufuatia zuio hilo baadhi ya wafanyabiashara wanaofanya biashara hiyo wamesema wameanza kuathirika kwani inawalazimu kuwashusha wageni na kutafuta usafiri mwingine kwenda na kutoka katika uwanja huo wa ndege.
Zuio hili la wafanyabiashara wa magari kutoka Tanzania wanaobeba na kupeleka wageni kwenye uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta kwa kiasi fulani huenda likatikisa uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia wa nchi hizo marafiki kama halitapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Credit; BBC
0 comments :
Post a Comment