Wakati CCM ikisubiri Februari kufanya tathmini kuona kama baadhi ya wagombea wake wa urais wametekeleza masharti ya adhabu zao, washindani wao wa Ukawa,
Jumanne ijayo watakutana kujadili mambo mbalimbali, ukiwamo mchakato wa kuwapata wagombea wake wa urais, ubunge na udiwani, imefahamika.
Tangu mwaka huu uanze zimekuwapo pilikapilika
nyingi za kisiasa ndani ya vyama vya siasa na Jumanne iliyopita CCM
ilifanya kikao cha Kamati Kuu mjini Zanzibar na kutoa maazimio
yanayogusia mchakato huo lakini ikasita kutaja ratiba rasmi ya mchakato
wa kuwapata wagombea wa CCM.
Wakati hali ikiwa hivyo, habari zilizopatikana na
kuthibitishwa na baadhi ya viongozi wa Ukawa, umoja huo utakutana jijini
Dar es Salaam Januari 20, ukiwa na ajenda mbalimbali kuhusu ushirikiano
wao, likiwamo suala la kupata wagombea huku vikao vya ndani ya vyama
vikitarajiwa mwishoni mwa mwezi huu.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia
alithibitisha jana kuwapo kwa kikao hicho Jumanne akisema kutakuwa na
ajenda nyingine lakini: “Suala la kupata wagombea nalo huenda
likajadiliwa. Kuhusu suala la mgombea urais wa Ukawa, linaweza kuwa
sehemu ya mazungumzo lakini halipo kwenye ajenda.”
Ajenda nyingine alizotaja ni mwongozo wa Ukawa,
kura ya maoni ya Katiba, changamoto za uandikishaji wa daftari la
wapiga kura, hali ya uchumi na tathmini ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
uliomalizika Desemba mwaka jana. Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi alisema watajadili ajenda hizo ili kuhakikisha wanatafuta
majibu ya changamoto zilizopo kwa sasa.
Kiongozi huyo pia alithibitisha taarifa kuwa kila
chama ndani ya Ukawa kupitia vikao vyake kitateua majina ya wagombea
ambao watashindanishwa ndani ya umoja huo, akisema kabla ya Machi, jina
la mgombea urais ndani ya chama chake litakuwa limeshapendekezwa.
Awali, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena
Nyambabe alisema vikao vya chama hicho vinavyotarajiwa kufanyika
mwishoni mwa mwezi huu vitakuwa na ajenda ya uchaguzi vitakavyojadili
mwelekeo wa uchaguzi huo kama kalenda yake inavyosema.
Credit; Mwananchi
Credit; Mwananchi
0 comments :
Post a Comment