ESCROW; VIGOGO WA TRA,BoT,TANESCO KIZIMBANI

Wahusika katika sakata la Escrow wakitinga katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam wakiongozwa na polisi na mawakili
Meneja Misamaha ya Kodi TRA, Kyabukoba Leonard Mutabingwa ,  Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco,  Steven Roman Urassa  na  Mkurugenzi wa fedha BOT , Julius  Rutta  Angello wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya kuomba na kupokea rushwa ya mamilioni ya fedha kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.

Watuhumiwa hao wanafanya idadi ya waliofikishwa mahakamani kwa kashfa ya miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow kufikia watano baada ya watumishi wengine wawili wa umma kufikishwa mahakamani Jumatano iliyopita.
Waliofikishwa mahakamani hapo ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma aliwekewa kiasi cha Sh323 milioni kupitia akaunti yake namba 00120102602001.
Mwingine ni Mhandisi Mkuu wa Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), Wizara ya Nishati na Madini, Theophillo Bwakea aliyepokea rushwa ya Sh161,700,000 kupitia akaunti yake namba 004101102643901.
Mahakama ya Kisutu leo
Washtakiwa hao wanaokabiliwa na mashtaka ya kuomba na kupokea rushwa  kinyume na kifungu cha 15 (1)(a) cha sheria ya kupambana na rushwa  namba 11 ya mwaka 2015, walifikishwa  kwa mahakimu wawili tofauti, Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda na Hakimu Mkazi, Devotha Kisoka.
Akisoma hati ya mashtaka katika kesi namba 16 ya 2015 inayomkabili Kyabukoba,   Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai   alidai mbele ya Hakimu Kaluyenda kuwa Januari 27, 2014 katika Benki ya Mkombozi  wilaya ya Ilala , alipokea Sh1.6 bilioni kupitia akaunti namba 00110202613801.
Swai alidai  kuwa mshtakiwa huyo akiwa katika Benki ya Mkombozi alijipatia kiasi hicho cha fedha  ambacho ni  sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow na kwamba alizipokea kutoka kwa James Burchard Rugemalira  ambaye ni Mshauri huru wa Kitaalam, Mkurugenzi wa VIP Engineering na Mkurugenzi wa zamani wa IPTL kama tuzo kwa kuiwakilisha kampuni ya  Mabibo Beer Wines and Spirits ambayo ni mali  ya Rugemalira  mahakamani  kitu ambacho ni kinyume cha sheria.
Alidai kuwa Julai 15, 2015, mshtakiwa huyo Kyabukoba  akiwa  katika benki hiyo ya Mkombozi alipokea rushwa ya Sh161.7 milioni, Agosti 26,2014 alipokea tena rushwa ya Sh 161.7 milioni na  Novemba 14, 2014 alijipatia rushwa ya kiasi kingine cha fedha cha Sh161.7 milioni kupitia kwenye akaunti hiyo, kama tuzo kwa kuiwakilisha kampuni hiyo ya  Rugemalira mahakamani kitu ambacho ni kinyume cha sheria na kwamba  fedha zote hizo ni sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Kyabukoba aliyakana na upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo umekwisha kamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya mshtakiwa huyo kusomewa maelezo ya awali (PH).



Credit; Mwananchi
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment