Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Salva Rweyemamu akiongea na waandishi wa habari. |
Ikulu imewataka Watanzania kuacha kulichukulia suala la kujiuzulu kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kama jambo la ‘kufa na kupona’, huku ikieleza kuwa waziri huyo mpaka sasa bado ni kiongozi wa Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema hatua
zilizochukuliwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim
Maswi aliyesimamishwa kazi kupisha uchunguzi haziwezi kuwa sawa na za
Profesa Muhongo kwa sababu Maswi ni mtumishi wa Serikali na profesa huyo
ni mwanasiasa.
Rweyemamu alitoa ufafanuzi huo baada ya kubanwa na
wanahabari waliotaka kujua sababu za Profesa Muhongo licha ya kuwekwa
kiporo na Rais Jakaya Kikwete kutokana na kuhusishwa na kashfa ya
uchotwaji wa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow, bado
anafanya shughuli mbalimbali za Serikali, ikiwa ni pamoja na juzi kwenda
kuhudhuria mkutano nchini Uswisi.
“Utaratibu wa kumwajibisha yeye (Muhongo) ni
tofauti na wa Maswi. Kama mtakumbuka Bunge lilitoa maazimio yake ambayo
bado yanaendelea kutekelezwa. Msilichukulie suala hili kama la kufa na
kupona,” alisema Rweyemamu.
Akizungumzia kauli hiyo, Mbunge wa Ubungo
(Chadema), John Mnyika alisema, “Kauli hiyo ya Ikulu inadhihirisha
udhaifu wa Rais. Rais alisema anamweka kiporo kwa siku mbili, Ikulu
inapaswa kueleza ni kwa nini Rais ameamua kumweka kiporo zaidi ya siku
hizo mbili wakati alidai kuwa kuna uchunguzi mdogo tu.
“Kwa namna wanavyomlinda Muhongo na watuhumiwa
wengine, naendelea kutoa wito kwa wabunge wenzangu tusaini hoja ya
kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kwa kuwa kwa kufanya hivyo, baraza la
mawaziri litavunjika na hivyo kiporo cha Muhongo na mizigo mingine ndani
ya baraza la mawaziri itaondoka.”
Katika kikao cha 16 na 17 cha Bunge, Bunge kupitia
azimio lake la pili liliazimia kwamba Waziri wa Nishati na Madini,
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi
ya Wakurugenzi wa Tanesco wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka yao ya
uteuzi kutengua uteuzi wao.
Kati ya wote waliolengwa katika azimio hilo ni
Profesa Muhongo pekee ambaye mpaka sasa bado hajawajibishwa na mamlaka
yake ya uteuzi.
Jaji Frederick Werema ambaye alikuwa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali alijiuzulu, Maswi alisimamishwa kazi, Profesa Anna
Tibaijuka aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
alifutwa kazi huku Bodi ya Tanesco ikiundwa nyingine.
Credit; Mwananchi
Credit; Mwananchi
0 comments :
Post a Comment