MAANDAMANO DHIDI YA MATUMIZI YA NGUVU YA POLISI YAONGEZEKA

Waandamanaji mjini New York na miji mingine wameandamana kwa usiku wa tatu jana Ijumaa(05.12.2014), wakishutumu matumizi ya nguvu yanayofanywa na jeshi la polisi dhidi ya jamii ya wachache.

Waendesha mashitaka hata hivyo wamesema wanafikiria kumfungulia mashtaka afisa aliyemfyatulia risasi mtu mmoja Mmarekani mweusi ambaye hakuwa na silaha Novemba mwaka huu.
Kifo cha Akai Gurley, mwenye umri wa miaka 28, aliyepigwa risasi katika maeneo yasiyo na taa za kutosha katika kitongoji cha Brooklyn mjini New York, ni cha hivi karibuni kabisa kufanywa na polisi na kusababisha hasira ya umma nchini Marekani kwa kile wengi wanachodhani ni matumizi ya nguvu yenye misingi ya kibaguzi yanayofanywa na jeshi la kulinda amani.
Sigara za magendo zamfikisha kuzimu
Wimbi la wiki hii la hasira inayooneshwa kwa maandamano ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa ya amani lilianza Jumatano wakati jopo la wazee wa baraza katika mahakama kukataa kumfungulia mashtaka afisa wa polisi mzungu Daniel Pantaleo baada ya Eric Garner kijana mweusi mwenye umri wa miaka 43 baba wa watoto sita kukabwa na polisi hadi kufa.
Garner, ambaye hakuwa na silaha, alikamatwa kwa tuhuma za kuuza sigara kinyume na sheria katika mpambano na polisi katika kisiwa cha Staten Julai mwaka huu ambao uliokuwa ukirekodiwa katika video.
Uamuzi wa kumuondolea mashataka Pantaleo ulitangazwa siku tisa baada ya jopo kama hilo la wazee wa baraza mahakamani jimboni Missori kuamua kutomshitaki polisi mzungu kwa kumpiga risasi kijana mweusi ambaye hakuwa na silaha mwezi Agosti katika kitongoji cha St. Louis mjini Ferguson, na kusababisha ghasia kubwa kwa siku mbili ambapo kulikuwa na uchomaji moto majengo na magari.
Matumizi ya nguvu dhidi ya jamii ya wachache
Tena siku ya Alhamis mjini Phoenix, jimboni Arozona, mtu mwingine mweusi ambaye hakuwa na silaha alipigwa risasi na polisi mzungu baada ya kukamatana nae, na kusababisha maandamano mjini humo. "Serikali imetengeneza zimwi na sasa zimwi hilo linaranda hovyo," amesema Soraya Soi Free, mwenye umri wa miaka 45, muuguzi kutoka Bronx ambaye amekuwa akiandamana mjini New York.
Waandamanaji na waombolezaji wamekusanyika usiku wa Ijumaa kutoa heshima kwa Gurley , ambapo mazishi yatafanyika leo Jumamosi .




Credit; DW
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment