Kwa mujibu wa katiba ya chama hicho mwanachama anayeruhusiwa kugombea urais ni lazima awe kiongozi wa chama, wadhifa ambao unashikiliwa na Zitto ambaye hajafikisha umri wa kikatiba wa kugombea urais ambao ni kuanzia miaka 40. Kwa sasa ana miaka 39.
“Ikitokea hivyo (ACT ikapata mgombea urais, kutoka ndani au nje ya chama hicho), mimi natoka namwachia mtu mwingine na tumeshaamua hivyo, kwetu sisi tatizo siyo cheo. Tukipata mgombea urais leo nitampisha, sitakuwa kiongozi wa chama nitabaki kuwa mwanachama wa kawaida na mjumbe wa Kamati Kuu.”
Hata hivyo, alisema ili mtu huyo apate nafasi hiyo ni lazima aelewe malengo ya chama hicho kilichopata usajili wa kudumu Mei, mwaka jana.
“Tunataka mtu ambaye hata tukipata mabadiliko asiwe kikwazo cha hayo mabadiliko. Nasema hivi kwa sababu mnaweza kupata mtu mwingine kuwa kiongozi wa chama lakini baadaye anang’ang’ania na hataki kutoka,” alisema.
Alifafanua kuwa yeye bado ni kijana ana muda mrefu katika siasa na anaungwa mkono sehemu nyingi, hivyo hana haja ya kuharakisha katika kila jambo.
Hata hivyo, akizungumzia watu wa vyama vingine watakaojiunga na chama hicho alisema, “Kati ya watu watakaojiunga ACT au walioonyesha nia kutoka CCM au Ukawa hadi sasa hakuna ambaye ni mgombea urais.”
Alifafanua, “Sisi (ACT) tutasimamisha mgombea wetu wenyewe katika nafasi ya urais au tunaweza kumuunga mkono mgombea wa upinzani.
Alisema watafanya hivyo kwa sababu hawataki kuua matumaini ya nchi kupata Serikali inayotokana na vyama vya upinzani, “Pale ambapo tutaona ni lazima kuunga mkono wenzetu kuing’oa CCM madarakani tutafanya hivyo. Si kama tunajiunga Ukawa, hapana ni kwa sababu bado hatujawa na mazungumzo nao na kujua nini kitakachotuunganisha.”
0 comments :
Post a Comment