Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. |
Siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema kuwa nafasi hiyo ni kadhia na kazi ngumu, baadhi ya wanasiasa waliotangaza nia ya kuwania nafasi hiyo wamesema wanafahamu changamoto hizo na kwamba kauli hiyo inazidi kuwapa nguvu na hamasa ya kuendelea na mchakato huo
Wiki iliyopita, Rais Kikwete akiwa Marekani,
wakati akihutubia kwenye taasisi ya Wood Wilson International Center for
Scholars alielezea mafanikio na changamoto alizokumbana nazo wakati wa
uongozi wake wa miaka 10 unaomalizika Oktoba, mwaka huu na kusema:
“Wakati unaingia Ikulu unakuwa na shauku kubwa
sana pamoja na furaha ya ushindi, lakini hakika urais ni kadhia kubwa.
Ukipata fursa ya kuwa rais kwa awamu mbili kama mimi nadhani zinatosha
kabisa. Nimefanya mengi kwa nchi yangu atakayekuja ataendeleza
nilipoishia.”
Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja wakati makada wa CCM wakipigana vikumbo kuwania urais.
Miongoni mwa wanasiasa waliotangaza na waliotajwa
katika kinyang’anyiro hicho cha kurithi kiti kitakachoachwa wazi na Rais
Kikwete ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa
Nzega, Dk Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Uratibu), Stephen Wasira, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Pia wamo, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel
Nchimbi, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na aliyekuwa Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
0 comments :
Post a Comment