Chid Benz |
Mwanamuziki Rashidi Abdallah Makwaro ‘Chid Benz’(29) amekiri mashtaka matatu yanayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya kukutwa na dawa za kulevya, kifuu cha nazi na kijiko vinavyotumika kuvutia ama kunusa dawa hizo za kulevya,,
Chid Benz alikiri kufanya makosa hayo mbele
ya Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema baada ya kuiomba Mahakama imsomee tena
mashtaka yake hayo yanayomkabili.
Aliomba kusomewa mashtaka hayo yanayomkabili,
muda mfupi baada ya kesi yake kutajwa mahakamani hapo na Wakili wa
Serikali, Diana Lukendo kudai kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa,
upelelezi bado haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine kwa
ajili ya kuangalia kama utakuwa umekamilika ama la.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Chid Benz
alinyoosha mkono na kuiomba mahakama imsomee tena mashtaka
yanayomkabili, akasomewa na kukiri kuwa Oktoba 24,2014 katika Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere alikamatwa akiwa na gramu
0.85 za dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride zenye thamani ya Sh
38,638.
Alikiri kuwa siku ya tukio alikutwa akiwa na gramu 1.72 za dawa za kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Sh 1,720.
Pia, alikiri kukamatwa akiwa na vifaa vinavyounganishwa na matumizi ya kuvuta ama kunusa madawa hayo ya kulevya.
Baada ya kukiri mashtaka hayo yote matatu, Wakili
wa Serikali , Lukendo aliiomba mahakama kutoa ahirisho fupi ili waweze
kujiandaa na kumsomea maelezo ya makosa yanayomkabili. Hakimu Lema
alikubaliana na ombi hilo na kuiahirisha kesi hadi Februari 23,2015.
Awali, Chid Benz aliposomewa mashtaka hayo
yanayomkabili mahakamani hapo aliyakana yote na upande wa mashtaka
ulieleza upelelezi wa kesi bado haujakamilika ikaendelea kuahirishwa
hadi alipokiri makosa hayo.
Credit; Mwananchi
Credit; Mwananchi
0 comments :
Post a Comment