Shule za msingi Ukombozi na Nyankumbu zilizopo mjini Geita mkoani hapa, zipo hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kutokana na kukosa vyoo na msongamano mkubwa wa wanafunzi kwenye madarasa.
Hali hiyo ni kinyume na Sera ya Elimu ya Mwaka 2010 inayotaka mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia..
Shule hizo zilizopo ndani ya eneo moja, zina zaidi
ya wanafunzi 4,000, choo kimoja chenye matundu 14 na madarasa 16, huku
kila tundu likitumiwa na zaidi ya wanafunzi 200.
Wakizungumza shuleni hapo jana, wakuu wa shule
hizo, Mwalimu Richard Rwengusi na Maxmilian Amos walisema hali ni mbaya,
kwani shule hazina vyoo na zinakabiliwa na upungufu wa madarasa na
madawati.
“Shule ya Ukombozi pekee yake ina wanafunzi 1,792,
madarasa manane, matundu ya vyoo 14, ambayo hadi sasa yamejaa na
madawati 176, hivyo wanafunzi 1,616 wanakaa chini, huku Shule ya
Nyankumbu ikiwa na wanafunzi 2,022 na madawati 180,” alisema Mwalimu
Mkuu wa Ukombozi, Rwengusi.
“Hapa hali ya usalama kwa watoto na walimu ipo
hatarini, vyoo vimejaa na vimebomoka upana wa madarasa ni mdogo,
wanafunzi wanabanana na hewa hakuna,” alisema Maximilian.
Walimu wanena
Walimu wa shule hizo walisema wanapata shida
kufundisha zaidi ya wanafunzi 300 kwenye darasa moja kutokana na hewa
nzito, kelele na vumbi.
Kamati za shule
Viongozi wa kamati za shule hizo wanakiri uwapo wa
hali hiyo na kwamba, suala hilo tayari limefikishwa kwa uongozi wa
Halmashauri ya Mji wa Geita.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Magreth
Nakainga alikiri kuwapo tatizo, lakini alisema wameshindwa kulitatua
kutokana na ukosefu wa fedha.
Credit; Mwananchi
Credit; Mwananchi
0 comments :
Post a Comment