Zitto Kabwe

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) itawasha moto upya bungeni wakati itakaposoma ripoti maalumu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikitarajiwa kuibua kashfa tatu nzito ikiwamo ya misamaha ya kodi.

Kashfa nyingine zinazotarajiwa kuibuliwa kesho ni, ufisadi katika gharama za ujenzi wa jengo la watu mashuhuri (VIP) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na uuzaji wa nyumba ya Bodi ya Korosho.
Habari zilizofika na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe zilisema kuwa, tayari kamati hiyo imepokea ripoti ya ukaguzi huo ambayo inaonyesha ufisadi wa kutisha katika maeneo hayo matatu na mengineyo.
Masuala hayo matatu pia yaliibuka wakati wa vikao vya kamati za Bunge vilivyomalizika Dar es Salaam wiki iliyopita, huku bodi ya korosho ikibanwa kuhusu nyumba yake aliyouziwa Mbunge wa Kibaha Mjini (CCM), Silvestry Koka.
Kwa mujibu wa habari hizo, ripoti hiyo inayoonyesha jinsi ufisadi wa kutisha ulivyofanywa katika ujenzi wa jengo la (VIP Lounge) na Serikali inadai ilitumia Sh12 bilioni kulijenga, lakini mthamini wa majengo ya Serikali ameeleza kuwa jengo hilo lina thamani ya Sh3 bilioni.
Katika suala la misamaha ya kodi, PAC imepokea taarifa kutoka kwa CAG ikionyesha kuwa misamaha hiyo iliyokuwa imefikia Sh1.5 trilioni mpaka Juni 2013, lakini baada ya mwaka moja misamaha hiyo imeongezeka hadi Sh1.8 trilioni mpaka Juni 2014.
“Kwa mwaka mmoja tu, misamaha ya kodi imeongezeka kwa zaidi ya Sh300 bilioni. Kiasi hiki ni kama escrow fulani (Fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, Sh306 bilioni),” chanzo cha habari kilidokeza.
Katika vikao vya kamati hiyo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilieleza kuwa misamaha ya kodi imepanda kutoka Sh1.4 trilioni mwaka 2012/13 hadi Sh1.8 trilioni mwaka 2013/14, chanzo kikiwa ni misamaha ya kodi katika miradi mikubwa. Ilisema kati ya misamaha hiyo, Sh676 bilioni zinatokana na misamaha ya kodi inayotokana na Ongezeko la Thamani (VAT) na kuwa hali hiyo itapungua iwapo nchi itaanza kutumia Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Pia, TRA ilifafanua kuwa mpaka sasa wafanyabiashara na kampuni kubwa zimefungua kesi katika mahakama ya rufaa wakipinga kulipa kodi ambayo inafikia Sh1.7 trilioni.
Mvutano mwingine unaotarajiwa kuibuliwa katika ripoti hiyo ni uwasilishwaji wa utata wa uuzwaji wa nyumba  ya Bodi ya Korosho.
Awali, hati ya nyumba hiyo ilikuwa ya Taasisi ya Kilimo Tanzania ambayo ilifutwa mwaka 1963, kabla ya mtu mwingine kuibadilisha hati na kuiuza kwa Koka mwaka 2011.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mudhihir Mudhihir alisema Koka aliuziwa nyumba na taasisi hiyo ambayo haikuwa mmiliki halali.




Credit; Mwananchi
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment