Zaidi ya watu 323 wakazi wa Kijiji cha namba 9 katika Kata ya Bulyanhulu wilayani Kahama mkoani Shinyanga, wanahofiwa kula sumu kali aina ya sodium cyanide inayotumiwa katika Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu unaomilikiwa na Kampuni ya Acacia.
Hali hiyo imetokana na mvua kubwa kunyesha na
kubomoa bwawa kubwa la ndani ya mgodi huo wa Bulyanhulu, ambalo hutunza
sumu hiyo na kusababisha maji hayo kutiririkia kwenye bwawa la nje
linalotumiwa na wananchi.
Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Acacia, Necta Foya alisema jana kuwa, maji hayo yalibomoa pia bwawa la nje na kwenda vijijini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya
Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya alisema baada ya maji hayo
yanayosadikiwa kuwa na sumu kubomoa bwawa la nje yalisambaa pia kwenye
mashamba ya watu.
Mpesya, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kahama,
alisema katika eneo hilo takriban hekta 15 za mpunga zimeathiriwa na
sumu hiyo, zikiwamo bustani za nyanya.
Mpesya alisema ili kunusuru maisha ya wananchi
hao, huduma zote za maji ya kunywa mifugo na binadamu kwenye visima na
mabwawa zimefungwa na tayari mgodi huo umevuta kwa muda maji ya bomba
ambayo sasa wananchi hao wanayatumia.
Hata hivyo, Mpesya alisema tayari watalaamu wa
afya na mazingira wamechukua sampuli ya maji hayo pamoja na nyanya
kwenye bustani inayodhaniwa kunyonya maji yenye sumu hiyo na kupeleka
Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali
Pamoja na hali hiyo, jana wananchi wote wanaoishi
eneo hilo walipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Kahama kupimwa afya zao,
zoezi ambalo lilikuwa likiendelea kufanywa na
madaktari wote kutoka halmashauri tatu za Wilaya ya Kahama.
Alisema uamuzi huo wa kuwapima wananchi unatokana kuhisi kuwa wametumia maji yaliyochanganyika na sumu hiyo.
Pia, Mpesya alisema kamati yake ilikubaliana na watu
hao wapimwe wakati hatua nyingine zikiendelea kufanywa ikiwa ni pamoja
na kusubiri majibu kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kujua sumu
hiyo imeingia kwenye eneo hilo kwa kiasi gani.
Credit; Mwananchi
Credit; Mwananchi
0 comments :
Post a Comment