Spika wa bunge la Tanzania Anne Makinda. |
Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema hawatambui wenyeviti wa kamati tatu za kudumu za Bunge ambao Bunge liliazimia wavuliwe nyadhifa zao kutokana na kutajwa katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Pamoja na kuwapo kwa maagizo hayo ya Bunge, baadhi yao
wanaendelea kujinasibu kuwa bado ni wenyeviti huku mmoja wao akiongoza
vikao vya kamati.
Anne Makinda alisema
anachofahamu ni kuwa wenyeviti hao tayari wameshajiuzulu na kamati zao
zinatakiwa kufanya uchaguzi wa wenyeviti wengine.
Wanaotakiwa kuachia nyadhifa zao ni Victor
Mwabalaswa (Nishati na Madini), Andrew Chenge (Bajeti) na William
Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala), ambaye bado alikuwa
akiongoza kikao cha kamati hiyo.
Siku tano zilizopita Katibu wa Bunge, Dk Thomas
Kashilillah alieleza kuwa kamati hizo zinatakiwa kufanya uchaguzi na
kwamba wenyeviti hao hawakutakiwa kuongoza vikao, lakini
hakuna uchaguzi wowote uliokuwa umefanyika na baadhi ya viongozi wanaendelea na
majukumu yao.
Katika mkutano wake wa 16 na 17, Bunge katika
azimio lake la tatu, liliazimia kuwa watu walioshiriki katika kashfa ya
miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow wakiwamo viongozi wa kamati hizo
tatu, wachukuliwe hatua kabla ya kuanza kwa mkutano wa 18 wa Bunge
unaotarajiwa kuanza Januari 27.
Ngeleja alikaririwa hivi karibuni
akisema kwamba anaendelea kushikilia nafasi hiyo kwa maelezo kuwa
uchunguzi sakata hilo bado unaendelea na ikithibitika ndipo Bunge
litachukua uamuzi ambao alisema atakuwa tayari kuutekeleza.
Credit; Mwananchi
Credit; Mwananchi
0 comments :
Post a Comment