huyu ndiye Zena mama wa mtoto ambaye ameathirika na madawaya kulevya |
Mtoto mwenye umri wa miezi mitatu, mkazi wa Buza, Dar es Salaam amebainika kuwa mwathirika wa dawa za kulevya ambapo damu na mkojo vya mtoto huyo vilichukuliwa na kupimwa katika maabara
ya Hospitali ya Mwananyamala na baada ya saa mbili, majibu yalitoka na kuthibitisha kwamba alikuwa na chembechembe za dawa za kulevya aina ya heroini.
Taarifa za kitabibu zinaonyesha kuwa kuwapo kwa
heroini mwilini mwa mtu, huweza kuonekana katika mkojo ndani ya siku
mbili hadi nne iwapo dawa hizo zilitumiwa na mhusika kwa kati ya saa
mbili hadi tano.
Hatua ya kumfanyia vipimo mtoto huyo wa kiume,
inatokana na jitihada za gazeti la mwananchi kutaka kufahamu jinsi utumiaji wa
dawa za kulevya kwa wanawake wajawazito na wale wanaonyonyesha
unavyoweza kumwathiri mtoto akiwa tumboni au anayenyonya maziwa ya mama
mwathirika.
Mtaalamu wa tiba katika Hospitali ya Mwananyamala,
Dk Elifasi Mritu anasema: “Ni kweli ukitumia dawa za kulevya wakati
unanyonyesha au wakati wa mimba, mtoto naye huathirika.”
Kauli ya Dk Mritu ambaye ni daktari katika kitengo
cha tiba ya methadone hospitalini hapo, inaungwa mkono na Mkuu wa
Kitengo cha Magonjwa ya Akili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),
Dk Frank Mushi ambaye anasema mama anayetumia dawa za kulevya akiwa
mjamzito humwathiri pia mtoto.
Mama wa mtoto azungumza
Mama wa mtoto, Zena maarufu Zerish, mkazi wa Yombo
Buza alikiri kwamba alipata ujauzito wakati akitumia dawa za kulevya na
kwamba hadi sasa anavuta dawa hizo huku akiendelea kumnyonyesha mtoto
huyo.
Anasema baada ya kujifungua hakukaa ndani kwa siku
40 kama wafanyavyo wanawake wengi wa Kitanzania, kwa sababu mwili wake
ulikuwa unahitaji ‘unga’ vinginevyo hali yake huwa mbaya.
Anasema baada ya kujifungua alianza kuzunguka huku
na kule akiwa na mtoto mgongoni, huku akiwa amebeba mfuko wake wa
plastiki wenye mahitaji muhimu ya mtoto kama nepi na nguo.
Anasema anapovuta au kujichoma dawa, mtoto wake
pia hupata ‘stimu’ kwa sababu hupata dawa hizo za kulevya kupitia maziwa
anayonyonya na hivyo wote wawili kulala fofofo sehemu yoyote ile.
Hata hivyo, kwa Zerish na mwanaye, anapofikia hali
ya kuwa ‘alosto’ (wakati dawa za kulevya zinapoisha mwilini na hivyo
kuhitaji tena), huwa ni adhabu kali mno.
Credit; Mwananchi
Credit; Mwananchi
0 comments :
Post a Comment