Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete. |
Rais Jakaya Kikwete amewataka wamiliki wa vyombo vya habari nchini kuwajengea uwezo waandishi wa habari kwa kuwapatia mafunzo kila mara, pamoja na kuboresha maslahi yao kwani wakishindwa kuwalipa vizuri, waandishi hao watalipwa na watu wa mtaani jambo ambalo linaweza kupunguza weledi
Rais Kikwete ameyasema hayo alipokuwa
akizindua rasmi kituo cha Televisheni cha Azam kinachomilikiwa na
Kampuni ya Said Salim Bhakresa(SSB) huku akimmwagia sifa Mwenyekiti wa
Kampuni hiyo Said Salim Bakresa kwa kueleza kuwa uwekezaji alioufanya
utaongeza ushindani katika sekta ya habari.
Aidha amekitaka chombo hicho kuweka mbele maslahi
ya utaifa kwa kuchuja habari zinazotakiwa kutangazwa kwani hata
mashirika makubwa ya habari duniani kama vile BBC na CNN nao
wanazingatia utaifa wao kwanza.
“Tanzania ni moja ya nchi zilizofanya vizuri
katika kuhama kutoka kwenye mfumo wa habari wa analogia kwenda digiti
kwa ubora wa hali ya juu hivyo kuzinduliwa kwa Studio za Azam TV
kutaendeleza kuongeza ufanisi wa ubora wake,”Amesema Rais Kikwete.
Pia amesema sekta ya habari ni moja ya mhimili mkubwa
hapa nchini ambao kazi yake ni kuhakikisha kuwa suala la Demokrasia
linaendelea kukua na kuthaminiwa, hivyo Serikali itaendelea kusimamia
uhuru wa vyombo vya habari kwa kutunga sheria zisizo kandamizi.
Amesema ubora wa vipindi, teknolojia sahihi na
waandishi na watangazaji wenye weledi mkubwa utakuwa chachu katika
kuifanya Azam tv iweze kutoa bidhaa bora hivyo kuongeza ushindani .
Aidha amesema uwekezaji wa ndani kwa Mtanzania
unaleta heshima kwa Taifa la Tanzania ikiwa ni pamoja na kuongeza pato
la mtanzania na kupunguza adha ya ajira inayoendelea kukua kila siku
nchini.
"Siku zote penye bidii penye maarifa penye mipango
ya uhakika hakuna kisichowezekana, hawa jamaa wameanzia mbali sana
bidiii imewafanya wafikie mahali hapa walipo:- aliongeza, Tumezoe kula
vitu vya Azam, kunywa vitu vya Azam, kushabikia timu ya Azam na sasa
tutasikiliza Azam, hii ni kazi nzuri kwa taifa hili alipongeza Rais
Kikwete"
Amesema kampuni ya Said Salim Bhakres (SSB) ni
moja ya kampuni inayoongoza kwa kutoa ajira mbalimbali kwa watanzania
hapa nchini, pia wanaongoza katika kulipa kodi stahiki za mapato hivyo
kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kasi.
Aidha Rais Kikwete amewataka wafanyakazi wote wa
kampuni hiyo kuendelea kusimamia sera ya ubora wa bidhaa, hivyo hata
kwenye bidhaa ya utangazaji wajikite katika suala hilo la ubora.
0 comments :
Post a Comment