WATU 45 WAUWAWA WABUNGE WAPIGWA MABOMU YA MACHOZI

Kwa mujibu wa mashahidi, mashambulizi hayo yametokea kwenye kijiji cha Azaya Kura kilicho umbali wa kilomita 50 kutoka mji mkuu wa jimbo la Borno, Maiduguri.
Chifu wa kijiji hicho, Mallam Bulama, ameliambia shirika la habari kwamba hadi kufikia jioni ya jana walikuwa wameshahisabu miili ya watu 45 baada ya kumalizika kwa mashambulizi hayo.
Jimbo la Borno limekuwa kitovu cha mashambulizi ya Boko Haram. Tarehe 26 mwezi uliopita, kundi hilo liliwateka nyara wasichana na wavulana 30, wengine wakiwa na umri wa hadi miaka 11, na takribani imekuwa ikivamia maeneo kadhaa ya jimbo hilo kila siku. Mwezi Machi watu 29 waliuawa baada ya kutumiwa vipeperushi kuwaonya kuwa wangelishambuliwa.
Mmoja wa wanavijiji waliofanikiwa kukimbia mashambulizi ya hapo Jumatano, Mohammed Bukar, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba washambuliaji waliharibu zaidi ya nusu ya nyumba za kijiji chao, wakazichoma moto pikipiki 50 na gari nne kabla ya kuondoka na chakula na wanyama kadhaa.
Hayo yakitokea, kwenye mji mkuu wa Nigeria, Abuja, polisi ilitumia mabomu ya machozi kujaribu kuwazuia wabunge wa upinzani, ikiwa ni pamoja na spika wa bunge, kushiriki kwenye kura muhimu juu ya pendekezo la Rais Goodluck Jonathan kuongeza muda wa hali ya hatari katika eneo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, ambako kundi la Boko Haram limekuwa likiendesha shughuli zake za kigaidi.
Katika vurugu hizo, wabunge waliokuwa wanapingana na ombi hilo walitaka badala yake ipigwe kura ya kumuondosha Rais Jonathan.
Chama kikuu cha upinzani nchini humo kimesema Rais huyo anakwenda kinyume na katiba kwa kuongeza muda wa hali ya dharura, na kwamba serikali yake imeshindwa kabisa kukabiliana na Boko Haram.
Spika wa Baraza la Seneti, David Mark, sasa amesitisha vikao vya bunge hadi hapo Jumanne. Spika huyo alitangaza kwamba polisi walitumia mabomu ya machozi kuzuia wabunge hao kukutana, ambapo wabunge hao walijaribu kulivunja lango la bunge kuingia ndani.
Licha ya mabomu hayo ya machozi, baadhi ya wabunge walifanikiwa kuingia ndani. Muda mchache kabla ya hapo, spika huyo alitangaza kuacha kumuunga mkono Rais Jonathan na kuungana na upande wa upinzani.




Credit; DW
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment